Al-madrasat Annour Islamia

Al-madrasat Annour Islamia Contact information, map and directions, contact form, opening hours, services, ratings, photos, videos and announcements from Al-madrasat Annour Islamia, Education, Mikunguni/kwa juma pweza/utapoa, Unguja.

23/09/2023

HISTORIA FUPI NA KUMBUKUMBU. ZA SHEIKH MUHAMMAD MAJID

Sheik Mohammed Majid ambae ni mmoja wa maulamaa wa dini ya kiislamu waliokuwepo hapa Zanzibar katika kuitangaza dini ya Mwenyezi Mungu(Uislamu).

Sheikh Mohammed Majid ni miongoni mwa wanazuoni maarufu wenye maarifa makubwa ya dini ya kiislamu waliotangulia mbele ya haki ambao walikuwepo Zanzibar katika kuitangaza dini ya Mwenyezi mungu.

Sheikh Majid atakumbukwa maisha kutokana na uwezo wake na kipaji alichojaaliwa na Mwenyezi Mungu katika kulingania dini ya Kiislamu na kuisambaza kupitia njia tofauti ili iwafikie wale waliokusudiwa.

Mohammed Majid alizaliwa Juni 5 mwaka 1956 katika kijiji cha Matemwe Mkoa wa Kaskazini Unguja,ambapo elimu yake ya awali alianza kuipata kisiwani Pemba kijiji cha Mchakaeni.

Sheikh Mohammed Majid alikuwa akiishi kisiwani humo kutokana na baba yake kuhamia kwa shughuli za uvuvi akitokea kijijini kwao Matemwe.

Mwaka 1965 alihamia kisiwani Zanzibar na kuanza elimu yake ya Maahad Islamia ambayo kwa sasa inajulikana k**a Chuo cha Kiislamu Mazizini ambapo kwa wakati huo ilikuwa ni elimu ya sekondari.

Mara baada ya kumaliza elimu ya sekondari Sheikh huyo alikwenda nchini Sudan mwaka 1984 katika chuo kikuu cha kimataifa cha Afrika kuchukua elimu ya dini ya kiislamu pamoja na lugha ya kiarabu .

Baadae alikwenda nchini Saudi Arabia kuchukuwa shahada ya kwanza ya dini ya Kiislamu na Kiarabu.

Mwaka 1992, alirudi Sudan kuchukua shahada ya Uzamili yaani ‘Masters Degree’ ya lugha ya Kiarabu na dini ya Kiislamu na mara baada ya kumaliza elimu hiyo alirudini nyumbani Zanzikbar.

Sheikh Mohammed Majid hakuwa nyuma katika maswala ya kutafuta elimu ya dini nay a dunia kutokana na kwamba alikuwa akijua umuhimu wa elimu.

Alikaa Zanzibar kwa muda mfupi na baadae alirudi nchini Sudan kuchukuwa elimu ya udaktari wa Falsafa “PHD” ya dini ya Kiislamu pamoja na lugha ya Kiarabu.

Elimu alizozipata nchi mbali mbali na aliyoipata hapa nchini kupitia walimu waliomsomesha dini aliweza kuongeza dini kipaji chake na kuwa na hamu kubwa ya kuitangaza dini ya kiislamu.

Dr Mohammed Majid baada ya kumaliza elimu hiyo na kurudi nyumbani alisomesha lugha ya Kiarabu katika kituo cha Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni ambacho kwa sasa ni Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA).

Pia Dk Mohammed Majid ni miongoni mwa waanzilishi wa Chuo Kikuu cha Elimu ya Kiislamu Chukwani na pia aliwahi kuwa msaidizi Mwalimu Mkuu Madrassat Noor mpaka mwaka 2000 baada ya kufariki marehemu Maalim Bakathir.

Sheikh Mohammed Majid alitawazwa rasmin kuwa mwalimu mkuu wa Madrassa hiyo iliyopo katika mtaa wa Ukutani mjini Unguja.

Mnamo mwaka 2002 sawa na mwaka 1423 Sheikh Mohammed Majid alifariki dunia na kuzikwa kijijini kwao Matemwe Mnazimmoja Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Dk Mohammed Majid atakumbukwa maisha na waislamu wote wa hapa visiwani Unguja na Pemba kwa ujumla kwa kuwa na changamoto kubwa ya kuanzisha kipindi cha Jiongezee Maarifa kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Zanzibar(ZBC).

Kipindi hicho kimeweza kuvutia vijana wengi kutaka kuifahamu na kusoma zaidi mwenendo wa dini yao ya kiislamu pamoja na kitabu kitukufu cha Quraan.

Baadhi ya masheikh waliokuwepo hapa Zanzibar wanamzungumzia kwamba atakumbukwa sana katika kipindi chake hicho cha Jiongezee Maarifa ambacho hupendwa na waislamu wengi kwa kuwafanya vijana wengi kuwa na hamu ya kuijua dini yao.

Sheikh Mohammed tunamkumbuka kwa mambo mengi mema aliyoyafanya wakati alipokuwa yuhai kwa kuanzisha kipindi cha Jiongezee maarufa ambacho kimewaongoa vijana wengi wa Kiislamu na kufanya kipindi hicho kikauwa mpaka kufikia kisiwani Pemba.

Katika kipindi hichi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani Sheikh Mohammed Majid alikuwa akisomesha somo la Fiqhi na Quraan katika msikiti wa Jongeani na msikiti wa Mchangani yote ya mjini Unguja.
ameweza kujijengea jina lake kwa kuweza kuitangaza dini ya Kiislamu kupitia Nyanja mbali mbali kwa vijana na watu wazima ili kuzidi kukuwa kwa jamii ya Kiislamu kwa kufuata maadili mema ya dini yao.

Aidha atakumbukwa kwa mambo mengi mazuri mbali ya kulingania dini ya Kiislamu,lakini pia mapenzi yake kwa watu wote wa rika tofauti,ucheshi na pia hakuwa mtu mwenye majivuno.

Shekh Muhammad Majid aliacha wake watatu na watoto 11,wanawake 10 na mwanamme mmoja.

Kwa niaba ya makala haya na mafundisho yake mema ya hapa duniani kwa ajili ya Akhera, Mwenyezi Mungu amsameh makosa yake na amlaze mahali pema peponi Aamin.

13/06/2023
17/02/2023

Assalam Alaykum warahmatullah wabarakatuh

TAARIFA KWA WAISLAMU WOTE WANAWAKE

Siku ya Jumamosi Tarehe 18,Febuary 2023 sawa na Tarehe 26 Rajab, 1444 .H

Wanawake wote wa kiislamu mnataarifiwa Dua Maalumu ya Kuombea Nchi iwe salama na Amani pamoja na kuwaombea ndugu zetu wa Uturuki 🇹🇷na syria 🇸🇾waliopata mtihani wa Tetemeko la ardhi mwaka huu 2023.

Wananchi wote wa Umma wa kiislamu wanawake mjitokeze kwa wingi kuiombea Nchi na yetu n.k

Dua itafanyika Michenzani nyuma ya block no 5 Chuoni kwa Marehemu Maalim Bi mkubwa Stadi Al- Madrasat Majalis Sania ,Dua hio itaongozwa na Ukhti Bi Sania Mahmoud Maalim muda wa saa 10:00 Za Alaasir

Walimu, wazazi wote pamoja na wanafunzi mnatakiwa kuhudhuria Dua hii muhimu

Taarifa hii mjuulishe na mwengine

Shukran
Imetolewa na Bi Sania Mahmoud

08/06/2022

*BM 4/4/7 MLANGO WA UGAWAJI WA ZAKA YA LAZIMA*

*Hadithi za Leo, Jumatano, tarehe 8, Dhul-Qa’da, 1443, sawa na tarehe 8, Juni 2022*

*KUHUSU UGAWAJI WA ZAKA YA LAZIMA*

*SEHEMU YA SABA*

*642-* وَعَنْ سَالِمِ بْنِ عَبْدِ اَللَّهِ بْنِ عُمَرَ، عَنْ أَبِيهِ; { أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ ﷺ كَانَ يُعْطِي عُمَرَ اَلْعَطَاءَ، فَيَقُولُ: أَعْطِهِ أَفْقَرَ مِنِّي، فَيَقُولُ: "خُذْهُ فَتَمَوَّلْهُ، أَوْ تَصَدَّقْ بِهِ، وَمَا جَاءَكَ مِنْ هَذَا اَلْمَالِ، وَأَنْتَ غَيْرُ مُشْرِفٍ وَلَا سَائِلٍ فَخُذْهُ، وَمَا لَا فَلَا تُتْبِعْهُ نَفْسَكَ". } رَوَاهُ مُسْلِمٌ .

*642.* Imepokewa kutoka kwa Salim bin Abdullah bin Umar *رضي الله عنه* kutoka kwa baba yake, Umar akisema: “Mtume ﷺ alikuwa anapomgawia kitu Umar, Umar alikuwa akijibu: "Mpe ambaye anaihitajia mali hiyo zaidi kuliko mimi.” Mtume ﷺ humwambia: “Chukua na itumie utakavyo au itoe sadaka. Na chochote kitachokujia kwa njia hii, pasi na wewe kuitazamia au kuiomba, kipokee na si lazima ukitumie wewe; unaweza kumgaiwa mtu mwingine. Venginevyo usiisumbue nafsi yako kukitafuta!” Ameipokea Muslim.

*UFAFANUZI*

Hadithi hii, inayo tufungia mlango huu wa Ugawaji wa Zaka ya lazima, inatufudisha kuwa ukipewa zawadi, si zaka wala si sadaka ya kujitolea, basi ipokee hata k**a wewe huihitajii zawadi hiyo. Kwani kukataa zawadi ni kumvunja moyo mtu aliye kutunikia. Chochote utacho pewa, bila ya kukiomba, wala kukitazamia na kukivizia,, kipokee midamu ni kitu halali na kinatoka kwa ndugu yako Mwislamu. Na iwapo hukihitajii, basi kwanza kipokee na mshukuru aliye kutunukia zawadi hiyo, na kisha mgawie mtu mwengine. Lakini usimvunje moyo aliye kutunukia. Ila usijushughulishe kuomba kitu ili ukitumie mwenyewe au ili ukawagaie watu wengine. Ukifanya hivyo unaingia katika makatazo tuliyo fundishwa katika Hadithi mbali mbali zilizopita, zenye kukataza na kukema ombaomba pasi na dharura ya kisheria. Hivyo, k**a una hamu na shauku ya kutoa sadaka na wewe huna kitu, basi katafute ajira au jitume ujichumie chumo la halali na kisha ujikimu mwenyewe na watu wako au utoe sadaka kutokana na chumo lako mwenyewe la halali. Kwa maneno mengine, Hadithi hii inasisitiza uharamu wa kuomba bila ya sababu ya msingi wa Kisheria katika Uwislamu, kwa upande mmoja, na kwa upande wa pili inasisitiza Uhalali, bali Sunna ya kupokea zawadi, bila ya kuiomba. Na kwa maana hiyo ukaraha mkubwa kukataa kupokea zawadi uliyo pewa na ndugu yako Mwislamu. Kwani kuingiza furaha kwenye moyo wa ndugu yako Mwislamu ni sadaka kubwa: *إدخال السرور على قلب المسلم صدقة*

*YALIYOMO NA YATOKANAYO*

1. Uhalali, bali ni sunna, kupokea zawadi kutoka kwa ndugu yako Mwislamu, hata k**a huihitajii zawadi hiyo.

2. Makuruhu sana kumvunja moyo ndugu yako Mwislamu aliye kutunukia zawadi ya halali.

3. Kumfurahisha ndugu yako Mwislamu ni sadaka.

4. Kujuzu kwa kiongozi wa Umma au kiongozi wa jamii kutoa zawadi kwa baadhi ya wanajamii kutokana na mali ya Umma.

5. Kujuzu, bali ni sunna, kwa mwanajamii wa Kiislamu kupokea zawadi kutoka kwa kiongozi wa jamii, bila ya kuitazamia wala kuiendea mbio ili apewe.

6. Ukaraha mkubwa kutumia mbinu za aina yoyote ili kiongozi wa Umma akugaiwe kitu, pasi na wewe kustahiki, kutoka kwenye mali ya Umma.

7. Kutumia mbinu ya aina yoyote ili upewe usichojuzu kupewa ni haramu; ni udanganyifu na wizi wa hila kutoka kwenye mali ya Umma.

8. Mwenye kumhadaa Mwenyezi Mungu anajihadaa nafsi yake.

9. Kujuzu kumgawia mtu mwengine kitu ulichopewa, iwe umepewa k**a zawadi tu, au k**a sadaka au hata k**a zake; hakuna junaha: na utapata ujira husika.

10. Haijuzu kuomba ili ukatowe sadaka au ukatowe zaka.

11. Ukaraha mkubwa wa kuvikodolea macho au kuvitaka vitu viliyomo kwenye mikono ya watu wengine. Chanzo cha husuda hicho.

12. Fadhila za Sayyidina Umar bin Al-Khattwwab *رضي الله عنه*.

*MWISHO WA KITABU CHA ZAKA*

والله أعلم

وبالله التوفيق

*Jiunge na mojawapo wa kumbi za DARSA za kila siku, pamoja na Maswali na Majibu, kutoka kwa Sayyid Abdulqadir Shareef, kwa kutuma MAOMBI yako, moja kwa moja, kwenda 0786887887, KUPITIA WHATSAP! Taja majina yako halisi MATATU, na MAHALI ulipo!*

Hifadhi *DARSA HII* ndani ya simu yako ili uweze kumtumia mwenzako! ‎

*من السيد عبدالقادر شريف آل الشيخ أبى بكر بن سالم*

Imetayarishwa na Sayyid Abdulqadir Shareef

Kutoka Kitabu cha _Ufikiaji wa Malengo kupitia Dalili za Hadithi za Fiqhi ya Milango_, kitabu ‎ambacho ni tafsiri kamili ya Kitabu kiitwacho: ‎*بلوغ المرام من أدلة أحاديث الأحكام* ‏‎ ‎kilichotungwa na Imam *الحافظ إبن حجر العسقلانى* na kufasiriwa kwa ‎Kiswahili na ‎Sayyid ‎Abdulqadir Shareef Aalish- Shaykh Abi Bakr bin Salim.‎

NI RUHUSA KUNUKUU, k**a ilivyo, pasi na kubadilisha au kuongeza chochote, ‎na ‎kuweka kwenye FB yako, ‎WhatsApp, na kwenye Makundi ‎ya ‎Mitandao ya Kijamii za Kiislamu, ‎kwa lengo la kusambaza na ‎kuelimisha ‎Dini. Changia kusambaza ‎Dini, ujipatie thawabu.

[email protected]

02/02/2022

*BM.28\28 MLANGO WA MASUALA YA MAITI*

*Hadithi za Leo, Jumatano, tarehe 30 Jumadal Akhira, 1443, sawa na tarehe 2, Februari, 2022*

*KUHUSU MLANGO WA JENEZA*

*SEHEMU YA ISHIRINI NA NANE*

*565-* وَعَنْ سَالِمٍ, عَنْ أَبِيهِ رضي الله عنه { أَنَّهُ رَأَى اَلنَّبِيَّ ﷺ وَأَبَا بَكْرٍ وَعُمَرَ, يَمْشُونَ أَمَامَ الْجَنَازَةِ. رَوَاهُ اَلْخَمْسَةُ، وَصَحَّحَهُ ابْنُ حِبَّانَ, وَأَعَلَّهُ النَّسَائِيُّ وَطَائِفَةٌ بِالْإِرْسَالِ.

*565.* Imepokewa kutoka kwa Salim رضي الله عنه kutoka kwa baba yake akisema: “Nimemuona Mtume ﷺ na Abubakar na Umar wanapo-kwenda kuzika wanatembea mbele ya jeneza.” Wameipokea Maimamu watano na ameisahihisha Ibn Habban lakini Nasai ameitia ila kidogo katika riwaya yake, vile wanazuoni wengine wa Hadithi wamesema maelezo hayo ni mursal.(yaani ni maelezo ya Swahaba si maneno ya Mtume ﷺ )

*UFAFANUZI*



Hadithi hii inatufundisha kuwa utaratibu bora wa kusindikiza maiti, ni kutembea mbele ya jeneza, yaani kulitangulia jeneza mbele kidogo, na kwamba hivyo ndivyo alilvyo kuwa akionekana Mtume ﷺ kufanya na ndivyo vile vile walivyo onekana Makhalifa wake wawili, Sayyidina Abu Bakr na Sayyidina Umar wakifanya. Riwaya ya Ibh Hibban kutoka kwa Az-Zuhry inawataja Makhalifa watatu wa Mtume:

*وَأَخْرَجَهُ ابْنُ حِبَّانَ فِي صَحِيحِهِ عَن الزُّهْرِيِّ عَنْ سَالِمِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عُمَرَ: كَانَ يَمْشِي بَيْنَ يَدَيْهَا وَأَبُو بَكْرٍ وَعُمَرُ وَعُثْمَان*

Imepokewa kutoka kwa Az-Zuhry kutoka kwa Salim bin Abdillah bin Umar akisema: “(Mtume ﷺ) alikuwa akitembea mbele ya jeneza, na Abu Bakr na Umar na Uthman.”

Vyovyote iwavyo, Hadithi inasalia kuwa si maneno ya Mtume ﷺ bali ni maelezo yanayo nasibishwa kwa Ibn Umar, na hivyo bado ni Hadithun Mursal. Kutokana na ukweli huo, wanazuoni wametofautiana kuhusu ubora ni upi katika kutembea kusindikiza maiti kwenda kuzikwa.



Kwanza kutembea mbele ya jeneza ndio bora –k**a ilivyo kuwa safu iliyo bora, zaidi, ikatika swala ya jamaa ni safu mwanzo – basi vile vile sehemu bora ya kusindikiza jeneza ni kuwa mbele ya jeneza husika. Ila wote wanapata thawabu. Msimamo huu ndio wa wanazuoni wengi, miongoni mwao ni Imam Shafii رحمه الله. Dalili yao ni Hadithi ya hapo juu, kwa hoja kwamba Ibn Umar hawezi kusema jambo k**a hilo kutoka kichwani mwake tu, na kwa maana hiyo maelezo ya Swahaba kwamba amemuona Mtume ﷺ akifanya jambo fulani ni sawa sawa na Hadithi ya matamshi au kitendo cha Mtume ﷺ : *له حكم الرفع* .

Pili: wanazuoni wengine, k**a Imam Abu Hanifa, wanaona kuwa kutembea nyuma ya jeneza, kwa mtindo wa kusindikiza, ni bora zaidi. Hoja yao ni Hadithi iliyopokewa kutoka kwa Ibn Twauus kutoka kwa Baba yake:

*رَوَى ابْنُ طَاوُسٍ عَنْ أَبِيهِ: مَا مَشَى رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ حَتَّى مَاتَ إِلاَّ خَلْفَ الْجِنَازَةِ، وَلِمَا رَوَاهُ سَعِيدُ بْنُ مَنْصُورٍ مِنْ حَدِيثِ عَلِيٍّ رضِيَ اللَّهُ عنهُ قَالَ: الْمَشْيُ خَلْفَهَا أَفْضَلُ مِن الْمَشْيِ أَمَامَهَا." إسْنَادُهُ حَسَنٌ، وَهُوَ مَوْقُوفٌ لَهُ حُكْمُ الرَّفْعِ.*

Imepokewa kutoka kwa Ibn Twaus kutoka kwa Baba yake akisema: “Mtume ﷺ hajapata kusindikiza jeneza, hadi kufa kwake, isipo kuwa kwa kutembea nyuma yake.” Riwaya nyengine ni kutoka kwa Said bin Mansuur, kutoka kwa Aliyy bin Abi Twalib akisema: “Kutembea nyuma ya jeneza ni bora kuliko kutembea mbele yake.” Isnad yake ni nzuri, ila bado ni Hadithun Mursal, yenye *حكم الرفع*, yaani sawa sawa na Hadithi ya Ibn Umar.

Kauli ya tatu ni kwamba ubora upo katika kusindikiza jeneza, iwe kwa kutembea mbele yake, nyuma yake, kuliani kwake au kushotoni kwake. Lilio muhimu ni kusindikiza maiti hadi kumzika. Dalili ya msimamo huu ni Hadithi inayo toka kwa Anas bin Malik رضي الله عنه – ambayo Imam Bukhari ameiweka katika ufafanuzi wa mlango wa Hadithi, ila Ibn Abi Shayba na Abdurrazzaq wameipokea kwa Isnadi kamili hadi kwa Mtume ﷺ :

*أَنَّهُ يَمْشِي بَيْنَ يَدَيْهَا وَخَلْفَهَا، وَعَنْ يَمِينِهَا وَعَنْ شِمَالِهَا، عَلَّقَهُ الْبُخَارِيُّ عَنْ أَنَسٍ، وَأَخْرَجَهُ ابْنُ أَبِي شَيْبَةَ مَوْصُولاً، وَكَذَا عَبْدُ الرَّزَّاقِ. وَفِيهِ التَّوْسِعَةُ عَلَى الْمُشَيِّعِينَ، وَهُوَ يُوَافِقُ سُنَّةَ الإِسْرَاعِ بِالْجِنَازَةِ، وَأَنَّهُمْ لا يَلْزَمُونَ مَكَاناً وَاحِداً يَمْشُونَ فِيهِ؛ لِئَلاَّ يَشُقَّ عَلَيْهِمْ، أَوْ عَلَى بَعْضِهِمْ (سبل السلام)*

“Msindikizaji anaweza kutembea mbele ya jeneza, au nyuma yake, au kuliani kwake au kushotoni kwake; k**a alivyo ipokea Bukhari katika kufafanua Hadithi ya mlango mahasusi kutoka kwa Anas, vile vile imepokewa na Abdurrazzaq. Zaidi ni kwamba katika kupendekeza pande zote hizo ni kuwapa wasaa na ukunjufu wasindikizaji wa maiti, na wakati huo huu kufanya hivyo kunaendana sana na Sunna ya kutakiwa tuharakishe kutembea na jeneza, na kwa maana hiyo wasindikizaji hawatalazimika kutembea sehemu moja tu na kuacha sehemu nyengine. Vile vile ni kufanya usindikizaji wa maiti uwe mgumu na mashaka juu ya wasindikizaji wote, au juu ya baadhi yao.” _Subulus-Salaam._

Yote haya ni kwa wasindikizji wa kutembea kwa miguu, ama wasindikizaji wanaopanda vipando vyovyote vile, basi wasindikize juu ya vipando vyao wakiwa nyuma ya wanao wanao tembea kwa miguu. Kuna Hadithi swahihi kutoka kwa Al-Mughira bin Shu’ba yenye kupendekeza hivyo:

*رَوَى الْمُغيرَةُ بنُ شُعبةَ مَرفوعاً: ((الرَّاكِبُ خَلْفَ الْجَنَازَةِ)). رواهُ التِّرمذيُّ (1031) وصَحَّحَهُ*

Imepokewa kutoka kwa Al-Mughira bin Shu’ba kutoka kwa Mtume ﷺ akisema: “Mwenye kupanda kipando asindikize nyuma ya jeneza.” Ameipokea Tirmidhi, H., 1031, n kuiswahihisha.

*YALIYOMO NA YATOKANAYO*

1. Wajibu wa kutoshelezana kusindikiza maiti hadi makaburini.

2. Kila msindikizaji atembee aonavyo bora kwake yeye, iwe mbele ya jeneza, nyuma ya jeneza, pembeni ya jeneza na kadhalika.

3. Inapendekezwa kwa waja wema na wachamungu watangulie mbele ya jeneza; kufanya hivyo ni sawa kumuombea msamaha kwa vitendo, kwa kutangulia mbele ya jeneza.

4. Sunna kusindikiza jeneza kwa kutembea kwa miguu, lakini hakuna junaha kusindikiza kwa kupanda vipando.

5. Ni wazi kuwa wanao sindikiza kwa kupanda vipando, k**a magari, wasindikize nyuma ya wanao tembea kwa miguu.

والله أعلم

وبالله التوفيق

*Jiunge na mojawapo wa kumbi za DARSA za kila siku, pamoja na Maswali na Majibu, kutoka kwa Sayyid Abdulqadir Shareef, kwa kutuma MAOMBI yako, moja kwa moja, kwenda 0786887887, KUPITIA WHATSAP! Taja majina yako halisi MATATU, na MAHALI ulipo!*

Hifadhi *DARSA HII* ndani ya simu yako ili uweze kumtumia mwenzako! ‎

من السيد عبدالقادر شريف آل الشيخ أبى بكر بن سالم

Imetayarishwa na Sayyid Abdulqadir Shareef

Kutoka Kitabu cha _Ufikiaji wa Malengo kupitia Dalili za Hadithi za Fiqhi ya Milango_, kitabu ‎ambacho ni tafsiri kamili ya Kitabu kiitwacho: ‎بلوغ المرام من أدلة أحاديث الأحكام ‏‎ ‎kilichotungwa na Imam الحافظ إبن حجر العسقلانى na kufasiriwa kwa ‎Kiswahili na ‎Sayyid ‎Abdulqadir Shareef Aalish- Shaykh Abi Bakr bin Salim.‎

NI RUHUSA KUNUKUU, k**a ilivyo, pasi na kubadilisha au kuongeza chochote, ‎na ‎kuweka kwenye FB yako, ‎WhatsApp, na kwenye Makundi ‎ya ‎Mitandao ya Kijamii za Kiislamu, ‎kwa lengo la kusambaza na ‎kuelimisha ‎Dini. Changia kusambaza ‎Dini, ujipatie thawabu.

[email protected]

25/01/2022

*BM.28\22 MLANGO WA MASUALA YA MAITI*

*Hadithi za Leo, Jumaane, tarehe 22 Jumadal-Akhir, 1443, sawa na tarehe 25, Januari, 2022*

*KUHUSU MLANGO WA JENEZA*

*SEHEMU YA ISHIRINI NA MBILI*

555- وَعَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ:{ وَاَللَّهِ لَقَدْ صَلَّى رَسُولُ اَللَّهِ ﷺ عَلَى اِبْنَيْ بَيْضَاءَ فِي اَلْمَسْجِدِ } رَوَاهُ مُسْلِمٌ

*555.* Imepokewa kutoka kwa ‘Aisha رضي الله عنها akisema: “Naapa kwamba Mtume ﷺ aliwaswalia msikitini watoto wawili waliofariki wa Al-Baydhwa’.” Ameipokea Muslim.

*UFAFANUZI*

Hadithi hii, ambayo Mama Aisha ameisimulia huku akila kiapo, inathibitisha uhalali wa kumswalia maiti msikitini, kinyume na baadhi ya watu, khasa baadhi ya Taabiuun (wafuasi wa Maswahaba), walio kuwa wakisema kuwa haijuzu au makuruhu kumswalia maiti msikitini kwa kuchelea kutokwa na najsi na kuchafua msikiti, isipo kuwa kwenye eneo la wazi ambalo ni maalumu kwa swala za maiti na swala za Idi mbili. Mbali na kuapa kwa jina la Mwenyezi Mungu, tena kwa yamini ya kutilia mkazo: Kiapo, kilicho ambatanishwa na *اللام، وقد، للتوكيد* (Lamu na Qad), Mama Aisha amekula kiapo hicho kumaanisha kuwa jambo hilo lilitokea na yeye kuliona kwa macho yake. Bali hata kuwataja majina watoto hao katika riwaya nyengine kuwa ni:

*سهل وسهيل، أبناء وهب بن ربيعة، وأمهما: دعد بنت جحدم، من بني فه*ر

“Sahl na Suhayl watoto wa Wahb bin Rabi’a na mama yao ni Da’d bint Jahdam kutoka ukoo wa Bani Fihr.”

Hivyo, sababu kubwa iliyo mpelekea Mama ‘Aisha رضي الله عنها kusimulia Hadithi ya Mtume ﷺ kuwaswalia watoto hao wawili msikitini ni kuwa alipo fariki Sayyidina Sa’d bin Waqqas, mwaka 55 Hijri, akiwa ndiye Muhajir wa mwisho kufariki Madina, Mama ‘Aisha alisema aswaliwe kwenye msikiti wa Mtume ﷺ Madina, na yeye mwenyewe akashiriki katika Swala hiyo. Baadhi ya watu hawakupendezwa na ushauri huo. Hivyo, akasema kuwajibu:

*مَا أَسْرَعُ مَا أَنْسَى النَّاسَ وَاَللَّهِ لَقَدْ صَلَّى: «وَاَللَّهِ لَقَدْ صَلَّى رَسُولُ اللَّهِ - صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ - عَلَى ابْنَيْ بَيْضَاءَ فِي الْمَسْجِدِ.» رَوَاهُ مُسْلِمٌ*

“Mbona baadhi ya watu wasahaulivu sana! “Naapa kwamba Mtume ﷺ aliwaswalia msikitini watoto wawili waliofariki wa Al-Baydhwa’.”

Na huo ndio msimamo wa Jumhur ya wanazuoni wa Ahlus-Sunna wal-Jama’a, kinyume na msimamo wa Imam Abu Hanifa na Imam Malik bin Anas رحمهما الله ambao kwao wao ni Makuruhu sana. Baadhi ya wafuasi wao wamefika kusema kuwa Swala ya maiti msikitini haiswihi. Dalili yao kubwa ni Swala ya Mtume ﷺ kumswalia Mfalme Najashi, aliye fariki Uhabeshi, ambaye Mtume ﷺ alitangaza kifo chake Madina na kuwataka watu wafuatane nae kwenda kumswalia kwenye eneo la kuswaliwa maiti, nje ya msikiti. Ila hoja hiyo, k**a walivyo sema wanazuoni wengi, miongoni mwao Maswahaba wa Mtume, haina mshiko kwani siyo tu Mtume ﷺ amepata kuwaswalia maiti msikitini, bali Maswahaba wakubwa wakubwa waliswaliwa maiti msikitini, miongini mwao ni kuwa Sayyidina Umar bin Al-Khattwab رضي الله عنه alimswalia Sayyidina Abi Bakr As-Swiddiq رضي الله عنه kwenye msikiti wa Mtume ﷺ na Sayyidina Swuhayb alimswalia Sayyidina Umar bin Al-Khattwab msikitini vile vile, mbele ya Maswahaba wakubwa wakubwa walioshiriki, na hakuna hata mmoja aliye pinga au kukataza. Ibn Abi Shayba amepokea hadithi ifuatayo:

*إنَّ عمر صلَّى على أبي بكر في المسجد، وأن صهيباً صلَّى على عمر فى المسجد (رواه إبن أبى شيبة)*

“Umar alimswalia Abu Bakr msikitini, na Swuhayb alimswlia Umar msikitini.” Ameipokea Ibn Abi Shayba.

Ndiyo maana, maiti wengi wa Kiislamu wanaswaliwa misikitini. Na kwa maana hiyo, inajuzu kumswalia maiti kwenye uwanja mahasusi wa swala za maiti aunaoitwa: *المصلى* au *الجبانة* na inajuzu, vil vile, kumswalia maiti msikitini. Hakuna junaha.

*YALIYOMO NA YATOKANAYO*

1. Inajuzu, bali ni Sunna vile vile kumswalia maiti wa Kiislamu msikitini.

2. Mtume ﷺ, mara nyingi aliwaswalia maiti uwanjani, lakini amepata, vile vile, kuwaswalia baadhi ya maiti msikitini.

3. Hakuna uharamu wala ukaraha wowote kumswalia maiti wa Kiislamu msikitini.

4. Kumswalia maiti ni kumuomba Mwenyezi Mungu ni hivyo ni ibada, na msikiti ni mahali pa kuabudu.

5. Mtume ﷺ aliwaswalia watoto wawili wa Al-Baydhwa’, msikitni, mbele ya Maswahaba.

6. Haiwezekani kukiita kitendo alicho kifanya Mtume ﷺ kuwa ni makuruhu.

والله أعلم

وبالله التوفيق

*Jiunge na mojawapo wa kumbi za DARSA za kila siku, pamoja na Maswali na Majibu, kutoka kwa Sayyid Abdulqadir Shareef, kwa kutuma MAOMBI yako, moja kwa moja, kwenda 0786887887, KUPITIA WHATSAP! Taja majina yako halisi MATATU, na MAHALI ulipo!*

Hifadhi *DARSA HII* ndani ya simu yako ili uweze kumtumia mwenzako! ‎

من السيد عبدالقادر شريف آل الشيخ أبى بكر بن سالم

Imetayarishwa na Sayyid Abdulqadir Shareef

Kutoka Kitabu cha _Ufikiaji wa Malengo kupitia Dalili za Hadithi za Fiqhi ya Milango_, kitabu ‎ambacho ni tafsiri kamili ya Kitabu kiitwacho: ‎بلوغ المرام من أدلة أحاديث الأحكام ‏‎ ‎kilichotungwa na Imam الحافظ إبن حجر العسقلانى na kufasiriwa kwa ‎Kiswahili na ‎Sayyid ‎Abdulqadir Shareef Aalish- Shaykh Abi Bakr bin Salim.‎

NI RUHUSA KUNUKUU, k**a ilivyo, pasi na kubadilisha au kuongeza chochote, ‎na ‎kuweka kwenye FB yako, ‎WhatsApp, na kwenye Makundi ‎ya ‎Mitandao ya Kijamii za Kiislamu, ‎kwa lengo la kusambaza na ‎kuelimisha ‎Dini. Changia kusambaza ‎Dini, ujipatie thawabu.

[email protected]

16/01/2022

Like page Al- Madrasat Majalis Sania Bi Mkubwa Stadi kwa ajili ya Darsa za sheikh Shareef Abdul-qaderr

14/09/2021

*JE, INAJUZU KULIPA SWALA YA WITRI KWA MWENYE KAWAIDA YA KUISWALI USIKU?*

Nimeulizwa, NANUKUU:-
*Nina kawaida ya kusali witri usiku ,nimepitiwa na usingizi mpaka adhana na swala ya lfajiri imeingia,jee naweza kudwali witri kisha nikaswali alfajiri*

JIBU
BISMILLAH!

Ndiyo, inajuzu, ila si baada ya kuswali Alfajiri, bali ama kabla au baada ya kuchomoza Jua.
Mwenye kawaida ya kufanya amali yoyote usiku, akapitiwa na usingizi hadi kushindwa kuitekeleza amali hiyo katika wakati wake wa kawaida, mpaka akaamka kwa swala ya Alfajiri, basi inamjuzia kuitenda amali hiyo baina ya wakati wa kabla ya kuswali Swala ya Alfajiri –si baada yake- au baada ya kuchomoza Jua na kabla ya Swala ya Adhuhuri. Hivyo k**a uradi huo ni kisomo tu, basi anaweza kuusoma kabla au baada ya Swala ya Alfajiri, au hata asubuhi, na kabla ya kuswali Adhuhuri. Ama ikiwa uradi huo ni swala ya Witri, kwa mfano, basi anaweza kuiswali kabla ya Swal ya Alfajiri, lakini SI baada ya kuswali Swala ya Alflajiri; maana hakuna kuswali swala yoyote baada ya kuswali Swala ya Alfakjifi, hadi baada ya kuchomoza Jua. Hivyo, ama aswali Wirti yake kabla ya kuswali swala ya Alfajiri, au baada ya kuchomoza Jua, na kabla ya Swala ya Adhuhuri. Tusome Hadithi zifuatayo kwa pamoja:
عَنْ عُمَرَ بنِ الخطَّابِ رَضِيَ اللهُ عَنْه قَالَ: قَالَ رَسولُ اللهِ صلَّى اللهُ عليه وسَلَّم: «مَنْ نَامَ عَنْ حِزْبِه مَنَ اللَّيلِ، أو عَنْ شَيءٍ مِنْه فَقَرَأَه ما بين صَلاةِ الفجرِ وصلاةِ الظهرِ، كُتِبَ له كأنَّما قَرأَه مَنَ اللَّيلِ» رواه مسلم
Imepokewa kutoka kwa Umar bin Al-Khattwab رضي الله عنه akisema: Amesema Mtume ﷺ : “Ataye pitiwa na usingizi asiweze kutekeleza uradi wake au baadhi ya uradi wake, akausoma baina ya Swala ya Alfajiri na Swala ya Adhuhuri, ataandikiwa kana kwamba ameuosoma katika wakati wake wa usiku.” Ameipokea Muslim.
Nyengine:
عن أبى سعيد الخدري رضي الله عنه قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((مَن نام عن الوتر أو نسِيه فليُصلِّ إذا أصبح أو ذكر))؛ رواه الخمسة إلا النسائي
Imepokewa kutoka kwa Abu Said Al-Khudriyy رضي الله عنه akisema: Amesema Mtume ﷺ : “Ataye pitiwa na usingizi akashindwa kuswali Witri yake, au ataye sahau kuswali Witri yake (hadi akaamka baada ya kupita usiku) basi aiswali itapo ingia asubuhi (yaani baada ya Jua kuchomoza) au atapo ikimbuka.” Imepokewa na maimamu watao, isipo kukwa Nasai.
Asubuhi ni baada ya kuchomoza Jua, na hivyo SI Alfajiri. Na Mtume ﷺ yeye mwenyewe aliwahi kupitiwa na usingizi asiswali Witri, hivyo akalipa rakaa 11 baada ya kuchomoza Jua. Na hii ni kwa sababu swala ya Witri inaswaliwa usiku, haiswaliwi Alfajiri. Hivyo, ikikupita kutokana na kupitiwa na usingizi,, au ikiwa umesahau kusali Witri yako, usiku, hadi ukaamka alfajiri, basi unaweza kuilipa baada ya kuchomoza Jua, na kabla ya Kuingia wakati wa Adhuhuri. Ila kwa sharti, iwe ni kawaida yako kuswali Witri kila siku usiku. Si venginevyo. Na hiyo ndiyo maana ya URADI. Uradi ni amali yoyote ya kujitolea unayo ifanya kwa mtindo wa kawaida, katika wakti maalum, kwa utaratibu maalum; iwe kisomo cha Qur’ani, Adhkari, Swala na kadhalika. Ila k**a ni swala, basi usiiswali katika nyakati zinazo katazwa kuswali,k**a wakati wa Kukchwa Jua, hadi lichwe kikamilifu, na wakati wa kuchomoza Jua, hadi liinuke urefu wa k**a mkuki.

والله أعلم

وبالله التوفيق

*HIFADHI NDANI YA SIMU YAKO ILI UWEZE KUMTUMIA MWENZAKO!*‎ ‎

من السيد عبدالقادر شريف آل الشيخ أبى بكر بن سالم

Imejibiwa na Sayyid Abdulqadir Shareef

Kutoka Masuali na Majibu: *Nimeulizwa, NANUKUU:--* yanayo jibiwa kila siku kwenye kumbi za Darasa za Mitandaoni, za Sayyid ‎Abdulqadir Shareef Aalish- Shaykh Abi Bakr bin Salim.‎

NI RUHUSA KUNUKUU, k**a ilivyo, pasi na kubadilisha au kuongeza chochote, ‎na ‎kuweka kwenye FB yako, ‎WhatsApp, na kwenye Makundi ‎ya ‎Mitandao ya Kijamii za Kiislamu, ‎kwa lengo la kusambaza na ‎kuelimisha ‎Dini. Changia kusambaza ‎Dini, ujipatie thawabu.
[email protected]

Address

Mikunguni/kwa Juma Pweza/utapoa
Unguja
ZB/ANNOUR/PC/01

Website

Alerts

Be the first to know and let us send you an email when Al-madrasat Annour Islamia posts news and promotions. Your email address will not be used for any other purpose, and you can unsubscribe at any time.

Shortcuts

Share

Category