14/01/2026
UDUGU WA KIELIMU WAZIDI KUIMARIKA: KULIYYA AL-BARAKAH YAFANYA ZIARA MAAHAD IMAM SHAFII – TANGA
Tanga:
Katika kuendeleza mashirikiano ya kielimu na kidini, Chuo cha Kuliyya ya Qur’an na Duruus Islamiyya Al-Barakah kutoka Tandale, Dar es Salaam, kimefanya ziara rasmi katika Maahad Imam Shafii, Tanga.
Ziara hiyo imelenga kuimarisha udugu wa kielimu na kuendeleza uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya taasisi hizi mbili za Kiislamu, sambamba na kubadilishana uzoefu katika nyanja za elimu ya Qur’an na Duruus za Kiislamu.
Katika ziara hiyo, wanafunzi wa Maahad Imam Shafii wamepata fursa adhimu ya kuhamasishwa kujiunga na Chuo cha Al-Barakah kwa ajili ya kujiendeleza kimasomo, hususan katika fani ya Qur’an kwa mfumo wa Qira’at na Riwayaat, ambao ni msingi muhimu katika taaluma ya Qur’an Tukufu.
Akizungumza na wanafunzi, ujumbe wa hamasa umetolewa ukisisitiza kuwa changamoto za kielimu ni daraja la mafanikio, huku wanafunzi wakihimizwa kuwa na subira, uvumilivu na kumtegemea ALLAH katika safari yao ya elimu.
Aidha, wanafunzi wamekumbushwa kuwa fursa za kielimu hazijirudii mara nyingi, hivyo wametakiwa kuzitumia ipasavyo kwa bidii na juhudi kubwa ili kujijengea mustakabali bora wa kielimu na kidini.
Ziara hii ni sehemu ya juhudi endelevu za taasisi hizi katika kuhakikisha vijana wa Kiislamu wanapata elimu bora, madhubuti na inayojengwa juu ya misingi sahihi ya Qur’an na Sunnah.
Cc AL Burhan
Ibrahim Kimaro
Swaadiq Bin Mwesa