01/09/2026
Nikiwa nacheza na mtoto wangu, mara bila kudhamiria nikamgonga, akaanguka, akalia; akiwa analia nilijisikia vibaya sana, ndio niliumia moyoni; basi nikawahi kumchukua alipokuwa chini, wakati namwendea alisema akiwa na maumivu "Wewe sio baba yangu, hunipendi, umenigonga", ndani ya sekunde kadhaa nilijisikia vibaya kusikia neno hilo, lakini baada ya kukaa chini nikakumbuka kuwa ni "MTOTO"; hajui wala hamaanishi asemayo, na amepata uhuru huu wa kusema hivi kwa sababu "ANANIAMINI".
Basi nikamchukua, nikambeba, nikaenda naye dukani, nikanunua "CHECHE" akafurahi sana; wakati tunarudi, akaniuliza "BABA UNANIPENDA" ? ( tayari karudi kwenye mfumo ) !
Hili swali lilinipa kujiuliza maswali mengi ndani, ndio mengi kwa wakati mmoja; lakini katika yote, nilisikia Roho mtakatifu ananisemesha jambo; "Mwanao yupo kwenye kipindi cha kutaka kuthibitishiwa k**a kweli unampenda kwa "maneno na matendo yako", walakini anasikia maneno mengi kutoka kwa makundi mbalimbali ya watu...."
Wakati haya yanaendelea, tulifika nyumbani, nikapiga naye picha "selfie " , alafu nikamuuliza kutoka kwenye picha " Hivi unafanana na nani " ? , akajibu "NAFANANA NA WEWE BABA" ( huku nikijua lazima aseme hivyo, kwa kuwa humsikia mara nyingi mama yake na watu wengine wakisema Micholine anafanana na Mchungaji mno ) , Nikamwambia "MIMI NI BABA YAKO", Akajibu kwa furaha katika namna ya kuuliza "KWELI ?" , nikamwambia "NDIO NI KWELI KABISA" , Akanikumbatia, akasema "NAKUPENDA BABA", Nikamwambia "NAKUPENDA PIA MWANANGU".
Okay ..... Ipo hivi !
:-
1:- HUJENGWA KATIKA IMANI.
“Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu.”
— Wagalatia 3:26 (Biblia Takatifu)
NB:- Mahusiano yoyote hujengwa katika "IMANI" baina ya watu wawili au watatu. Imani hupitia vipindi mbalimbali ili ithibitishwe katika matendo.
2:- HUJENGWA KATIKA MUUNGANIKO WA ROHO.
“Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani, Baba.”
— Wagalatia 4:6 (Biblia Takatifu)
:-
“Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye.”
— 1 Yohana 3:1 (Biblia Takatifu)
________________________
Michael FOJ
Mwanza, Tanzania.
+255 (0) 757 129 776.