29/08/2026
WATUMISHI WA MOCU WAJENGEWA UWEZO KUHUSU ELIMU JUMUISHI NA MASUALA YA JINSIA
Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) kimeendesha mafunzo kuhusu Elimu Jumuishi na Masuala ya Jinsia, yaliyofanyika tarehe 28 Agosti 2026 katika ukumbi wa Weruweru Lodge, mkoani Kilimanjaro.
Mafunzo hayo yaliyowahusisha Watumishi wa Chuo yamefadhiliwa na Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) unaotekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Akifungua mafunzo hayo, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Prof. George E. Matto, alimpongeza Mratibu wa Masuala ya Jinsia(kupitia timu ya inayoratibu mradi huo - Chuoni), Dkt. Asteria Ngaiza, pamoja na wawezeshaji kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambao ni Dkt. Lulu Mahay na Prof. Sarah Kisanga, kwa kufanikisha mafunzo hayo.
Prof. Matto amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha washiriki kupata uelewa wa kuzuia na kukemea vitendo visivyofaa, pamoja na kuchukua hatua pale changamoto zinapotokea.
Amesisitiza kuwa ni wajibu wa kila mwanajumuiya ya MoCU kutumia maarifa anayopata katika kujenga mazingira yenye usawa, utu, heshima na ujumuishi.
Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa miongozo mbalimbali ya Serikali kuhusu elimu na masuala ya jinsia, na yamehitimisha awamu ya mafunzo yaliyokuwa yakitekelezwa kwa hatua tangu mwaka 2021, lengo likiwa ni kuendeleza uelewa na uwajibikaji wa Watumishi katika kukuza mazingira jumuishi ndani ya Chuo.