21/01/2021
Msemo wa "Kwio hiyo kwio."
Msemo huo ni maarufu sana Jijini Dar es Salaam. Msemo huo ulianza kupata umaarufu baada ya kutumika katika wimbo wa mwanasingeli Meja Kunta aliyeshirikiana na mwanabongo fleva aitwaye Lava Lava.
Msemo wa "kwio" au "kwio hiyo kwio" umetokana na mlio wa kuku "kishingo" ukipewa maana ya "kudharau na kupuuza jambo unaloelezwa au kutokubaliana nalo". Kwa mfano:
MTU 1: Ndugu, yangu nimenunua gari.
MTU 2: gari hilo kwio!
Msemo huo unaenda sambamba na msemo mwingine uitwao "kudanga" ukiwa na maana ya kuchepuka kimapenzi kufanya ngono na wapenzi tofauti kwa maslahi au makusudio anayojua mhusika. Ni wazi kuwa misemo hii imepata umaarufu sana kipindi cha mwaka mmoja tu uliopita.
Hata hivyo msemo huo wa "kwio" umeonekana kumkera zaidi Mh. Makamu wa Rais wa JMT, mama Samia na kutaka mabaraza ya kiswahili kushughulikia hilo. Je, yupo sawa? Si sahihi, kwa nini?
Lugha ni zao la jamii, na lugha moja huwa na vilugha ndani mwake k**a vile: msimu, rejesta, lahaja, kitabaka, kibinafsi na lugha rasmi. Kila kilugha huwa na wazangumzaji wake kutokana na mazingira husika. Hivyo kusema kilugha fulani kisitumike maana yake umesema hiyo jamii itoweshwe duniani au jamii fulani isiwepo. Kwa hiyo hata msemo huo "kwio" ukipigwa marufuku hautaweza kuzuia jamii husika kutumia au kuibua misemo (misimu) mipya. Kazi ya mabaraza ni kuchunguza misemo (maneno) hiyo na kuona k**a itafaa kurasimishwa. Yapo maneno mengi yaliyotokana na misimu k**a ilivyo leo neno la "kwio" na baada ya kudumu kwa muda mrefu yakapata kuhalalishwa, nayo ni:
Kasheshe
Mchakato (neno la kubuni)
Kupe
Beberu au bepari
Ngangari
Mkereketwa, n.k.
Hivyo misimu haizuiliki, ukitaka kuizuia basi fisha jamii yote, pasiwepo mtu.