11/05/2016
VITUKO DUNIANI
Mwanamke afutwa kazi kwa kutovaa viatu vya juu
Karani mmoja wa kupokea wageni mjini London alilazimika kurudi nyumbani baada ya kukataa kuvaa viatu vyenye visigino virefu,imebainika.
Mfanyikazi huyo wa kampuni ya Temp, Nicola Thorp mwenye umri wa miaka 27 kutoka Hackney aliwasili katika kampuni moja inayoshughulikia maswala ya kifedha PwC kabla ya kuarifiwa kwamba anahitajika kuvaa viatu vyenye visigino vya nchi 2 hadi 4.
Alipokataa na kulalamika kwamba mbona wenzake wa kiume hawakutakiwa kuvaa hivyo,alitakiwa kurudi bila ya mshahara.
Kampuni ya Portico imesema kuwa iliweka sheria hizo kwa wafanyikazi wanaokabidhiwa PwC lakini imesema kuwa haitaondoa sheria hiyo.
Walimu walipwa vifaranga badala ya mshahara Uzbekistan
Mji mmoja nchini Uzbekistan umekua ukiwapa waalimu wake kuku k**a mshahara badala ya pesa. Mamlaka za mji wa Nukus katika jimbo linalojitawala la Karakalpakstan wamekua wakitia vifaranga wachanga kwa walimu kutokana na uhaba wa pesa nchini humo.
Kituo cha radio kinachofadhiliwa na Marekani{Radio Ozodlik} kimemnukuu mwalimu mmoja akilaani hatua hiyo k**a aibu kubwa kwa mamlaka.
Mwalimu huyo aliyeghadhabishwa na hatua hiyo amesema hataki vifaranga kwa sababu anaweza kuwapata sokoni, lakini wanataka pesa zao.
Vifaranga wanaotolewa k**a mshahara wana gharama ya dola mbili kila mmoja, ikiwa ni maradufu bei inayouzwa vifaranga sokoni.
Mamlaka za Uzbekistan hazikubalii uhuru wa vyombo vya habari na raia wa huko hutegemea vyombo vya habari vya kimataifa kutoa sauti yao, ila hawajitambulishi.
Uzbekistan imekumbwa na uhaba wa fedha kwa miaka sasa hali inayosababisha serikali kuchelewesha mishahara ya wafanyikazi na malipo ya uzeeni.
Mapema mwezi huu wafanyikazi wa serikali katika mji mkuu,Tashkent walilalamikia kwamba hawakuwa wamelipwa mshahara kwa miezi miwili kwa sababu benki hazikuwa na pesa.
Mwanamke wa miaka 72 ajifungua mtoto India
Mwanamke wa umri wa miaka 72 amejifungua mtoto mvulana katika hospitali moja nchini India.
Mwanamke huyo alipachikwa mimba kupitia njia ya kitaalamu ya IVF ambapo yai la mwanamke hutolewa kutoka kwenye ovari, kutungishwa mbegu ya kiume na kisha kurejeshwa kwenye mji wa mimba. Yai hilo linaweza kutolewa kwa mwanamke mwingine.
Njia hiyo hutumiwa kuwawezesha wanawake tasa kupata watoto.
Daljinder Kaur alijifungua mtoto wake baada ya kupokea matibabu kwa miaka miwili katika hospitali iliyoko jimbo la Haryana.
Matabibu walifanikiwa kumtungisha mimba kupitia IVF mara yao ya tatu.
Mumewe Kaur ana umri wa miaka 79.
Kisa hicho kimezua mjadala mkali kuhusu kutumiwa kwa teknolojia hiyo ya IVF na umri ambao wanawake wanaweza kuruhusiwa kuitumia kupata watoto.
Dkt Kanad Nayar, katibu mkuu wa chama cha upachikaji mimba nchini India anasema sheria ya kuamua umri wa juu ambao mwanamke anaweza kuruhusiwa kutumia teknolojia hiyo itatungwa karibuni.
Sana umri huo utakuwa miaka karibu miaka 55.
Daktari huyo anasema jambo la kuzingatiwa zaidi ni uwezo wa mwanamke kumlea mtoto hadi akomae.
Ni mara ya pili kwa mwanamke mkongwe kujifungua mtoto India. Awali, mwanamke wa miaka 70 alijaliwa mtoto nchini humo.
Lakini mwanamke huyo alifariki miaka miwili baadaye na sasa mtoto huyo anatuzwa na jamaa zake.