14/05/2026
Chama cha Wataalamu wa Magonjwa ya Viungo na Misuli (Rheumatology) tarehe 14 Mei 2026 kimefanya Mkutano wa Sita wa Magonjwa ya Viungo na Misuli kwa Watoto Afrika katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), ukiwa na kaulimbiu “Upatikanaji wa Huduma za Afya kwa Wote: Tukiungana kwa Afya Bora ya Viungo.”
Mkutano huo umewakutanisha wataalamu wa afya, watafiti, watunga sera kutoka Afrika na maeneo mengine duniani kwa lengo la kuimarisha huduma za matibabu ya magonjwa ya viungo na misuli kupitia ubunifu, elimu na ushirikiano.
Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Dkt. Gunini Kamba aliwashukuru waandaaji kwa kuendelea kuhamasisha tafiti na utoaji wa huduma za magonjwa hayo, hususan kwa watoto. Alisema Wizara ya Afya inaendelea kutoa ufadhili na kuandaa wataalamu zaidi ili kuboresha huduma nchini Tanzania.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi kutoka MUHAS, Prof. Francis Furia, alisema bado kuna upungufu mkubwa wa wataalamu wa magonjwa ya viungo na misuli duniani, hali inayosababisha wagonjwa wengi kukosa huduma na uchunguzi sahihi kwa wakati. Aliongeza kuwa mkutano huo umewezesha wataalamu wa afya kupata mafunzo yatakayosaidia kuongeza uwezo wa utambuzi na matibabu ya mapema.
Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wataalamu wa Magonjwa ya Viungo na Misuli, Dkt. Ayodele Fayele, alisisitiza umuhimu wa serikali kuendelea kuwekeza katika mafunzo ya madaktari bingwa wa watoto pamoja na kuingiza huduma hizo kwenye mfumo wa bima ya afya ili kupunguza gharama za matibabu kwa wagonjwa.
Naye Prof. Karim Manji alisema ushirikiano wa wataalamu kutoka nchi mbalimbali za Afrika kupitia mtandao wa PAFLAR unapaswa kuimarishwa zaidi kupitia ufundushaji na mitaala ili kuongeza uelewa kwa jamii na kuboresha huduma za magonjwa ya viungo na misuli kwa watoto barani Afrika.