23/04/2021
Assalam Alaykum
Shukrani zote ni za Allah ( SW )
Rehema zimfikie Mtume wake (SAW)
Leo tutaendelea na fadhila za kumi la pili la mwezi mtukufu wa Ramadhani, ikiwa ni muendelezo wa darsa liliopita.
(2) KUMI LA MSAMAHA
Kumi la pili la mwezi wa Ramadhani ni masiku yaliyo bora zaidi kwa waumini kutokana na kuletewa karibu fursa ya kusamehewa makosa yetu yaliyotangulia.
Bila shaka Mwenyezi Mungu mtukufu ndiye mwenye kusifika kwa sifa ya kuwasamehe viumbe wake na amelieleza hilo katika aya nyingi ndani ya kitabu chake kitukufu.
Anasema Mwenyezi Mungu katika surat Nnajim 32
{ Hakika ya mola wako ni mwingi wa msamaha }
Bila ya shaka yoyote ile tunapata kuona ukubwa wa msamaha wa Allah kwa viumbe wake na amewataka wajitahidi kuomba msamaha zaidi kwakuwa yeye hatokuwa mchoyo wa kuwasamehe.
Hivyo tunatakiwa kuongeza bidii katika hili kumi la pili kwa kufanya ibada kwa wingi kutoa sadaka kwa wenye mahitajio pia kuwa karibu na mayatima na kuwatembelea wagonjwa na kuwasaidia katika matatizo waliyonayo huku tukiomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu kutokana na matendo tuliyoyafanya kwa kusahau au kwa kujua ubaya wake au kwa kutokujua.
Anasema Mtume Muhammad ( saw )
"Hakika Mwenyezi Mungu hachoki kutoa msamaha ikiwa watu hawatoacha kumuomba msamaha"
Hivyo basi tulitumie vyema hili kumi la pili katika kuhakikisha tunafutiwa dhambi zetu zote.
Allah atujaalie kuwa miongoni mwa viumbe vyake vinavyomtaka msamaha.
Itaendelea...!
Tumuombe Allah atukubalie funga zetu na atujaalie mwisho mwema.
Imeandaliwa na:-
Muswaw Wara Madrasa
(Kiwalani Minazi Mirefu)