07/02/2026
IRAN (WAAJEMI): URITHI WA ESTA NA MORDEKAI KATIKA HISTORIA YA KALE
Historia ya Esta (Esther) na Mordekai (Midekai) si hadithi ya mbali ya Biblia tu, ni simulizi iliyotokea ndani ya moyo wa Ufalme wa Waajemi (Persia), taifa linaloitwa leo Iran.
Wakati falme zikijiona zina nguvu, hadithi hii inaonyesha jinsi mamlaka ya kisiasa yalivyotumika bila kujua kutimiza kusudi la Mungu. Hii inadhihirishwa hadi hivi leo juu ya uthubutu, misimamo na nguvu ya Iran (Waajemi).
Matukio yalitokea Shushani (Susa), mji wa kifalme wa Waajemi uliopo Iran ya leo. Ndani ya jumba la kifalme, mwanamke Myahudi aliyekuwa hana sauti wala nguvu aligeuka kuwa Malkia, na sauti yake ikasimamisha hukumu ya maangamizi dhidi ya taifa zima.
Mordekai, Myahudi aliyeishi chini ya utawala wa kipagani, alikataa kuinama mbele ya mamlaka dhalimu. Ukaidi wake haukuwa wa kiburi, bali wa imani na msimamo wa haki. Ndani ya mfumo wa Waajemi, alisimama akijua hatima inaweza kuwa kifo, lakini historia ilimpa ushindi.
Sawa, nakiri kwamba Uajemi haikuwa falme ya Mungu, lakini ilitumika na Mungu.
Sheria zake, kasri zake na mihuri yake vilitumiwa kubadili hukumu ya mauti kuwa uhai. Hii ni hoja nzito kwamba, si kila falme inayotumiwa na Mungu inatoka katika falme za Mungu.
Hadithi ya Esta ni ukumbusho mkali kwamba nguvu za dunia zina mipaka, na kwamba wakati mwingine wokovu hutokea katikati ya mifumo ambayo haikuandaliwa kuwa rasmi mbele za Mungu, badala yake kwa mapenzi yake Mungu ameitumia mifumo hiyo.
Hadi leo, Purimu inaadhimisha ushindi huu, na Iran ya kale inabaki kuwa jukwaa la simulizi moja ya ujasiri mkubwa zaidi katika Biblia.
Kumbuka, historia haisimuliwi tu, bali inapangwa.
Na
Mwanahistoria
Dar, Tz