09/07/2022
"BRIGHT FUTURE KINARA WA MATOKEO JIJI LA DAR ES SALAAM."
Matokeo ya Kidato cha Sita yalitolewa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa ndugu Athumani S. Amasi mnamo tarehe 05 Julai 2022 katika ukumbi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali (WEMA)-Zanzibar . Baraza la Mitihani la Tanzania liliidhinisha kutangazwa rasmi kwa matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Sita (ACSEE) uliofanyika tarehe 09 - 27 Mei, 2022.
Shule ya Sekondari Wasichana Bright Future imeibuka kuwa Mshindi wa Kwanza(1) katika Mkoa wa Dar es Salaam na nafasi ya kumi na Nne (14) Kitaifa kwa ufaulu wa daraja la Kwanza na la Pili pekee.
Sambamba na hayo Shule imefanikiwa kutoa Mwanafunzi mmoja kuwa miongoni mwa Watahiniwa waliofanya vizuri zaidi Kitaifa upande wa Wasichana waliopatikana kwa kulinganishajumla ya pointi kwenye masomo ya Tahasusi (combination) pamoja na wastani wa alama za jumla walizozipata. Julitha Frolian Silangwa alipata daraja la kwanza kwa wastani wa alama tatu (3) kutoka Mchepuo wa PCM akipata Alama "A" katika masomo yote matatu na kushika nafasi ya 10 Kitaifa.
Shule ya Sekondari Wasichana Bright Future ni Shule ya Bweni kuanzia Kidato cha Kwanza mpaka kidato cha Sita, inayopatikana katika Kata ya Msongola, Wilaya ya Ilala katika jiji la Dar es Salaam ikiwa na Mazingira bora na rafiki kwa Mwanafunzi kuwezesha kujifunza.