31/03/2025
_*SIKU ROHO YANGU ITAKAPOKUWA INATOLEWA: TAFAKURI YANGU*_
✍️Abdillah Kitota (MMEDSC)
Ndugu msomaji, hakuna siku itapita bila kutafakari juu ya roho yangu. *NATAFAKARI:* roho yangu ni kitu gani? Sayansi yake ikoje? Ipo sehemu gani ndani ya mwili wangu? Imeenea mwili mzima au kuna sehemu fulani ya mwili imewekwa na inasambaza athari yake katika kila sehemu ya mwili k**a ilivyo kwa moyo? Inafananaje? Inashikika au haishikiki? Ni sehemu ya malighafi tuliyoumbiwa; k**a ilivyo kwa udongo na maji, au ni kitu kingine kabisa? Vipi itakavyokuwa ikitolewa mwilini mwangu? Nitahisi uchungu wa namna gani k**a inavyosemwa?
Maswali haya na mengine mithili ya haya yamekuwa yakinirejesha kwenye Qur'an na Hadithi/Sunnah kutazama kuwepo, ukubwa na utukufu wa Mola wangu Mlezi juu ya jambo hili.
Mara nikakutana na Hadithi iliyosimuliwa na sahaba Abdullah Ibn Mas'ud (Radhiya Llaahu 'anhu) na kuripotiwa katika rejea za Hadithi zinazotegemewa; zikiwemo sahihi mbili. Katika Hadithi hii, Abdullah Ibn Mas'ud (Radhiya Llaahu 'anhu) anasimulia:
Nilipokuwa natembea na Mtume Swalla Llaahu 'alayhi wasallam katika moja ya mashamba ya Madina huku amejiegemeza kwenye buwa la mtende, likapita kundi la Wayahudi huku wakisemeshana wao kwa wao: *muulizeni kuhusu roho,* wengine wakasema: msimuulize atawajibu majibu ambayo hayatawaridhisha. Baadhi yao wakasema: tutamuuliza. Hivyo, mmoja kati yao akasimama na kumuuliza: *O Abul Qasim roho ninini?*
Mtume Swalla Llaahu 'alayhi wasallam akakaa kimya kwa muda. Kisha akasoma: *Na wanakuuliza khabari za Roho. Sema: Roho ni katika mambo ya Mola wangu Mlezi. Nanyi hamkupewa katika ilimu ila kidogo tu (Qur'an, 17:85).*
Kwa majibu hayo kutoka kwa Mola wetu Mlezi Mtukufu, imenibainikia kwamba, *mwanadamu hakupewa elimu ya kufahamu roho ninini hasa [ni kitu gani na sayansi yake ikoje]?*
Niliposonga mbele kuisoma Qur'an zaidi na maelezo yaliyotolewa na baadhi ya wanazuoni wa Kiislamu [ambayo huenda nayo yanarejea nyuma mpaka kwa Mtume Swalla Llaahu 'alayhi wasallam], ikanibainikia kwamba, hata hivyo, tumebainishiwa ishara chache sana zinazodokeza kuhusu roho, *lakini siyo zinazobainisha au kudokeza roho ninini hasa, na sayansi yake ikoje?*
Pia ikanibainikia kwamba, roho siyo kitu cha kiumbo k**a vilivyo vitu vingine vya kiumbo; *mathalan udongo na maji,* ambavyo Mola wetu Mlezi Mtukufu alivitumia k**a malighafi [sababu] ya kumuumba mwanadamu. Kwa maneno mengine, roho siyo *mwili wa kiumbo (physical body)* [uliojengwa kwa mwili na viungo vyake, na sehemu ya mwili isiyoshikika ambayo ni zao la moyo; yenye uwezo wa kuusukuma mwili kwenye halali au haram (tafsiri nyingine ya nafsi)], *bali ni mwili wa kiroho [spiritual body] usioweza kuonekana hata kwa mashine maalumu za kuuscreen mwili.* Kwa mujibu wa tafsiri nyingine ya nafsi [ya uwakilishi binafsi]; hasa nilipoisoma Qur'an, 32:9, imenibainikia kwamba, nafsi ya mwanadamu imejengwa kwa vitu vikuu viwili: *mwili wa kiumbo na mwili wa kiroho.*
Kwa kuwa roho ni *mwili wa kiroho,* huenda ndiyo sababu Mola wetu Mlezi Mtukufu anapodokeza kuhusu kitendo cha kumpulizia roho mwanadamu, anainasibisha roho na Yeye Mwenyewe moja kwa moja; *tofauti na anavyoeleza kwa uwazi kabisa kuhusu malighafi hayo aliyoyatumia kumuumba mwanadamu.* Mathalan, kuhusu udongo, imekuja katika Hadithi iliyosimuliwa na Abdullah Ibn Mas'ud (Radhiya Llaahu 'anhu) na maswahaba wengine kwamba, *ulichukuliwa kutoka sehemu mbalimbali za ardhi.* Suala la roho kuwa kitu cha kiroho ambacho Mola wetu Mlezi Mtukufu anainasibisha na Yeye Mwenyewe limenibainikia kwa uwazi kabisa kupitia aya zilizoainishwa hapa chini:
فَإِذَا سَوَّيْتُهُ وَنَفَخْتُ فِيهِ مِن رُّوحِي فَقَعُوا لَهُ سَاجِدِينَ
*Na nitakapo mkamilisha na KUMPULIZIA ROHO INAYO TOKANA NAMI, basi muangukieni kwa kumt'ii (Qur'an, 38:72).*
ثُمَّ سَوَّاهُ وَنَفَخَ فِيهِ مِن رُّوحِهِ ۖ وَجَعَلَ لَكُمُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَالْأَفْئِدَةَ ۚ قَلِيلًا مَّا تَشْكُرُونَ
*Kisha akamtengeneza, na AKAMPULIZIA ROHO YAKE, na akakujaalieni kusikia na kuona, na nyoyo za kufahamu. Ni uchache mnavyo shukuru (Qur'an, 32:9).*
فَإِذَا سَوَّيْتُهُ وَنَفَخْتُ فِيهِ مِن رُّوحِي فَقَعُوا لَهُ سَاجِدِينَ
*Basi nitakapo mkamilisha na NIKAMPULIZIA ROHO YANGU, basi mumwangukie kumsujudia (Qur'an, 15:29).*
Ishara nyingine iliyonibainikia inayodokezwa kwenye aya hizo ni kwamba, roho imetajwa k**a kitu cha mwisho *kuwekwa* ndani ya mwili wa mwanadamu *baada ya mwili wa mwanadamu kukamilika kuumbwa.*
Al Imam Ibn Kathir katika kitabu chake *Qiswasw Al Anbiya* ameeleza namna roho ya baba yetu Nabii Adam ('Alayhis salaam) ilivyowekwa. Kwamba, ilianza kuingia kichwani, akapiga chafya, kisha malaika wakamwambia sema alhmdulillah, akasema alhamdulillah, Mola wetu Mlezi Mtukufu akamwambia: Mola wako Mlezi Amekurehemu. Roho ilipofika machoni, akaangalia matunda ya peponi, ilipofika kwenye fumbatio [abdomen] akapata hamu ya kula, akaruka haraka kufuata chakula kabla roho haijafika miguuni, ili ale matunda ya peponi. Kisha Al Imam Ibn Kathir akanukuu Qur'an, 21:37 ambapo Mola wetu Mlezi Mtukufu amesema: *mwanadamu ameumbwa na haraka.*
Nikaendelea kubainikiwa zaidi nilipoirejea Hadithi ya Abdullah Ibn Mas'ud (Radhiya Llaahu 'anhu); ambayo nayo ni muttafaqun 'alayhi, inayobainisha hatua za makuzi na maendeleo ya mwanadamu ndani ya mfuko wa uzazi mpaka kwenye kuandikiwa yale *mambo manne [matendo, ajali, riziki, na mnyonge au mbarikiwa].* Katika Hadithi hii, kitu cha mwisho pia kutajwa ni kupuliziwa roho.
Ikanibainikia pia kwamba, suala la roho ya baba yetu Nabii Adam ('Alayhis salaam) na roho zetu [watoto wake] *kuwekwa* mwishoni kabisa baada ya kukamilika kuumbwa, linadokeza ishara nyingine kwamba, roho ndiyo iliyokadiriwa kuwa sababu ya maisha halisi ya seli, makundi ya seli [tishu], viungo na mifumo yote ya mwili [ukiachana na reflex]. Kwa maana hii, huenda roho imeenea mwili mzima.
Ikanibainikia pia kwamba, ishara nyingine kuhusu roho inayodokezwa ndani ya Qur'an ni *kuhusu kutolewa kwake.* Qur'an inadokeza kwamba, roho inatolewa kwa muundo wa *kutokea chini kuja juu [bottom to the top]*; kinyume na roho ya baba yetu Nabii Adam ('Alayhis salaam) ilivyoingizwa *[juu kuja chini; top to the bottom].* Aya zifuatazo zinalibainisha hili:
كَلَّا إِذَا بَلَغَتِ التَّرَاقِيَ
*La, hasha! (Roho) itakapo fikia kwenye mafupa ya koo (Qur'an, 75:26).*
فَلَوْلَا إِذَا بَلَغَتِ الْحُلْقُومَ
*Yawaje basi itakapo fika roho kwenye koo (Qur'an, 56:83).*
Katika tafsiri ya Qur'an, 75:26, nikakuta kwamba, Al Imam Ibn Kathir anasema: *[wakati wa kifo] roho itavutwa nje ya mwili wako mpaka itafika kwenye mifupa ya koo [kabla ya kutolewa nje kabisa na kurudishwa kwa Mola wetu Mlezi Mtukufu].*
Nikabainikiwa pia kwamba, hapa kuna ishara zingine mbili zinazodokezwa kuhusu roho: ya kwanza, roho ni kitu kilichoenea mwili mzima [kwa sababu wakati wa kutolewa kwake inavutwa kutoka chini (miguuni) kuja juu; takriban sawa na kusema inavuliwa], na pili, kitendo hicho cha kuvutwa kwa roho kina ambatana na uchungu mkali sana wa kutolewa roho; na huenda kadiri inavyovutwa, sehemu ya chini ya mwili inakuwa ikipoa na kukoma maisha; kadiri mifumo ya mwili inavyozidi kucollapse *[the point of NO return].*
Haya ni miongoni mwa yaliyonibainikia. *Kwamba, siku roho yangu itakapokuwa inatolewa, itakuwa ikivutwa kwa muundo huo; huku uchungu ukiwa ni makali sana.*
Hata hivyo, *bado natafakari;* hasa kuhusu muundo huo wa kutolewa kwa roho [kuvutwa]. K**a kuvutwa huko kwa roho kutoka chini kuja juu kunauma sana, *huenda imebana sana, na huenda ikivutwa kwa nguvu uchungu unazidi kuwa mkali zaidi. Je! wakati roho yangu inatolewa [kifo], Mimi ni katika wanadamu watakaovutwa roho zao kwa nguvu. Au taratibu?*
*Kwa yakini, ni juu yangu MIMI na WEWE kutenda matendo yetu katika njia ya Mola wetu Mlezi Mtukufu k**a lilivyo lengo la kuumbwa kwetu; ili siku roho zetu zitakapokuwa zinatolewa zitolewe taratibu angalau kupunguza uchungu wa kutolewa roho. Japokuwa bado uchungu wake ni mchungu sana.*
Katika Sahih, imeripotiwa kwamba, wakati Mtume Swalla Llaahu 'alayhi wasallam akiwa kwenye uchungu wa kifo *[huku akijifuta jasho usoni],* alisema:
*Subhaanaka Llaah, inna lilmauti lasakarat [umetakasika Mwenyezi Mungu. Hakika mauti yana uchungu].*
Kwa hakika, suala la roho ni muujiza mkubwa sana. Unaotuonesha kwamba Mola wetu Mlezi Mtukufu Yupo, ni Mkubwa na ni Mtukufu. K**a Qur'an ilivyobainisha kuwa hatukupewa elimu kuhusu roho ninini hasa na sayansi yake ikoje, mpaka sasa hakuna mwanasayansi yeyote wa Biolojia au tiba ya sasa aliyejaribu japo kung'amua *asili ya roho [ni kitu gani hasa?], muda halisi wa kuwekwa kwake mwilini ndani ya mfuko wa uzazi na kwa utaratibu [mechanism] gani, na lini itatolewa na kwa utaratibu gani [lini mtu atakufa]?* Na hatatokea mwanasayansi atakayefahamu au hata kung'amua hakika hizi.
Hii ni ishara nyingine inayotubainishia kwa uwazi kabisa kwamba, Qur'an ni maneno halisi ya Muumba wa mbingu na Ardhi; *ambaye ndiye Muumba wa mwanadamu.*