17/07/2026
IAA YAHIMIZA TAFITI ZISITUNZWE MAKABATINI BALI ZIWALETEE WANANCHI SULUHISHO
Tafiti zinazofanywa katika taasisi za elimu ya juu, ikiwemo Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), hazipaswi kubaki kwenye machapisho au maktaba pekee, bali zinapaswa kusambazwa kwa jamii na wadau ili ziwe sehemu ya utatuzi wa changamoto katika sekta mbalimbali, ikiwemo kilimo.
Hayo yamesemwa leo, Julai 16, 2026, na mwakilishi wa Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu, CRN Charles Rafaeli, wakati akifungua warsha ya usambazaji wa matokeo ya utafiti kuhusu uundaji wa jukwaa la kujifunza kwa njia ya mtandao kwa kutumia akili unde (AI) katika kilimo cha vitunguu maji na vitunguu swaumu. Warsha hiyo ilifanyika katika ukumbi wa PGB wa IAA.
Aidha, amebainisha kuwaIAA imeendelea kuwekeza katika tafiti shirikishi, ubunifu, matumizi ya teknolojia za kisasa na kuimarisha ushirikiano na jamii ili kuleta matokeo chanya katika sekta mbalimbali, hususan kilimo, akiongeza kuwa jitihada hizo zinalenga kujenga uchumi shindani na kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa upande wake, Afisa Kilimo wa Wilaya ya Arusha, Mhandisi Chrisben Saria, aliwahimiza wakulima na wadau wa sekta ya kilimo kutumia vifaa vya kielektroniki, hususan simu janja, kujifunza teknolojia mbalimbali zinazosaidia kuongeza tija na kutatua changamoto katika uzalishaji wa mazao, ikiwemo vitunguu maji na vitunguu swaumu, akisema matumizi ya teknolojia za kidijitali yanaweza kuwasaidia wakulima kupata taarifa sahihi kwa wakati, kuboresha mbinu za uzalishaji na kuongeza mavuno.
Naye mtafiti mkuu na mhadhiri Godson Mshana amesema utafiti huo uliofadhiliwa na Mradi wa HEET umetekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili na miongoni mwa matokeo yake ni uundaji wa jukwaa la kujifunza kwa njia ya mtandao linalotumia akili unde (AI), lijulikanalo k**a PataIntel, ambalo litawawezesha wakulima na wadau kupata maarifa na taarifa kwa wakati kuhusu kilimo cha vitunguu maji na vitunguu swaumu.
.