11/04/2026
NGUVU YA MSAMAHA - Uponyaji wa Kiroho.
KIFUNGU: Waefeso 4:31–32
LENGO: Bila uponyaji wa ndani, hasa katika eneo la msamaha, huwezi kukua kiroho.
UTANGULIZI:
Ndugu zangu, k**a vile mwili usiotibiwa unapokuwa na ugonjwa hushindwa kukua vizuri, ndivyo ilivyo pia kwa roho ya mwanadamu. Mtu anaweza kuwa anaenda kanisani, anaomba na kusoma Biblia, lakini ndani yake kuna majeraha, chuki, uchungu na kutokusamehe. Hali hii inazuia ukuaji wake wa kiroho. Leo tutajifunza kwamba msamaha ni tiba ya kiroho, ni dawa ambayo Mungu ametupa ili kuponya mioyo yetu. Ulimwengu unasema ukisamehe wewe ni dhaifu au mjinga, lakini Biblia inafundisha kwamba msamaha ni nguvu, si udhaifu.
MSAMAHA NI TIBA YA MOYO ULIOJERUHIWA
A. Waebrania 12:15
B. Mtu aliyefanyiwa mabaya alitegemea wema lakini akarudishiwa ubaya. Anaumia na anaweka maumivu moyoni. Maumivu yenyewe ni tatizo, lakini kuyashikilia moyoni ni tatizo kubwa zaidi. Ni k**a kidonda kilichopona lakini kovu bado lipo; ukikikuna kinaanza kuuma tena.
C. Wakristo wengi wanabeba uchungu wa zamani na kusema “nimesamehe lakini sitasahau.” Huu si msamaha wa kweli. Msamaha wa kweli ni kuachilia adhabu na haki ya kulipiza kisasi. Unaposhikilia uchungu unajiumiza mwenyewe na unazuia uponyaji wako. Msamaha unakuponya wewe kwanza.
MSAMAHA SI UDHAIFU, NI NGUVU YA KIROHO
A. Mathayo 18:21–22
B. Yesu akiwa msalabani alisema, “Baba, wasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo.” Alikuwa katika maumivu makubwa lakini alichagua kusamehe.
C. Ulimwengu unasema ukisamehe wewe ni mjinga au dhaifu, lakini Yesu anaonesha msamaha ni nguvu ya juu ya kiroho. K**a msamaha ungekuwa udhaifu, Yesu asingetuambia tusamehe bila kikomo. Kadri unavyosamehe ndivyo unavyokuwa na nguvu zaidi kiroho.
MSAMAHA HUONDOA UDUMAVU WA KIROHO NA KULETA UKUAJI
A. Waebrania 8:12
B. Stefano alipokuwa anapigwa mawe alisema, “Bwana, usiwahesabie dhambi hii.” Hakuomba kulipiza kisasi bali aliomba msamaha kwa waliomuumiza.
C. Kutokusamehe kunapofusha macho ya moyo na kunazuia mtu kuona mapenzi ya Mungu. Kunazaa uchungu, hasira, chuki na fitina. Lakini msamaha hufungua macho ya moyo, huleta amani na ukuaji wa kiroho. Unaposamehe unafanana na Kristo na unaanza kuona njia ya Mungu katika maisha yako.
WITO.
Ndugu zangu, msamaha si chaguo bali ni Amri kwa Mkristo. Yesu alisamehe, Stefano alisamehe, na sisi tunaitwa tusamehe. Kumbuka kwamba msamaha ni tiba, ni nguvu na ni ufunguo wa ukuaji wa kiroho. Usiseme nimesamehe lakini sitasahau, bali sema nimeachilia na nimemwachia Mungu. Unapomsamehe mtu haumponyi yeye tu, bali unajiponya wewe mwenyewe. Leo chagua kuachilia, chagua kusamehe ili roho yako ipone na ukuaji wako wa kiroho uanze. Amina.