31/08/2026
SOMALIA KUNUFAIKA NA UZOEFU WA TPSC KATIKA KUANZISHA CHUO CHA TAIFA CHA UTUMISHI WA UMMA
Dar es Salaam, Agosti 31, 2026
Serikali ya Somalia imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha mageuzi ya utumishi wa umma kwa kujipanga kuanzisha Chuo cha Taifa cha Utumishi wa Umma huku ikilenga kutumia uzoefu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) katika uendeshaji wa taasisi ya mafunzo ya watumishi wa umma.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Shirikizo ya Somalia, Mhe. Hirsi Jama Ganni ulipotembelea Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) akiongoza ujumbe wa serikali hiyo ikiwa ni sehemu ya ziara rasmi ya siku nne nchini Tanzania iliyolenga kujifunza uzoefu wa Tanzania katika mageuzi ya sekta ya umma, mabadiliko ya kidijitali na maboresho ya mifumo ya Serikali.
Mhe. Ganni amesema Somalia imeweka mageuzi ya utawala wa umma kuwa moja ya vipaumbele vya kitaifa na kwamba mafanikio ya Serikali yanategemea kuwa na watumishi wenye ujuzi na uwezo wa kubadilisha sera na mipango kuwa matokeo halisi kwa wananchi.
“Somalia inapanga kuanzisha Chuo cha Taifa cha Utumishi wa Umma kitakachokuwa na jukumu la kutoa mafunzo kwa watumishi wa Serikali, kuanzia mafunzo ya awali kwa watumishi wapya hadi mafunzo kwa viongozi waandamizi. amesema Mhe. Ganni”
Akizungumzia ziara hiyo, Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa TPSC, Dkt. Ernest Mabonesho, amesema ujumbe huo umetembelea Tanzania kwa lengo la kujifunza namna utumishi wa umma unavyoendeshwa nchini, huku ziara ya TPSC ikiwa na msisitizo wa kujifunza kuhusu uanzishwaji na uendeshaji wa chuo cha utumishi wa umma.
Dkt. Mabonesho amesema Somalia ilikuwa na chuo cha utumishi wa umma hapo awali, lakini taasisi hiyo ilishindwa kuendelea kufanya kazi kutokana na changamoto zilizotokana na vita, hivyo sasa nchi hiyo inapanga kuanzisha upya taasisi hiyo kwa kujifunza kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania.