22/05/2026
Mkuu wa Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC), Bw. Aristid Kanje, amewataka wataalamu wa usalama wa viwanja vya ndege kutumia maarifa waliyopata kuongeza ufanisi kazini. Amesisitiza kuwa wao ni nguzo muhimu katika kuimarisha usalama wa usafiri wa anga kwenye ukanda huu
Bw. Kanje ametoa wito huo leo Mei 22, 2026 wakati akifunga mafunzo ya Maafisa Usimamizi wa Usalama wa Viwanja vya Ndege (Airport Security Supervisors) yaliyoendeshwa yakiendeshwa chuoni hapo kuanzia tarehe 18 Mei 2026.
Alisema usalama wa viwanja vya ndege ni msingi muhimu wa sekta ya usafiri wa anga, hivyo wataalamu hao wanapaswa kufanya kazi kwa umakini mkubwa katika kubaini, kuzuia na kukabiliana na changamoto za kiusalama kwa kutumia mbinu na maarifa ya kisasa waliyojifunza.
“Sekta ya usafiri wa anga inahitaji umakini wa hali ya juu. Nendeni mkatumie ujuzi mliojifunza kuimarisha usalama katika maeneo yenu ya kazi,” alisema Bw. Kanje.
Aidha, alibainisha kuwa chuo hicho kitaendelea kutoa mafunzo yenye viwango vya kimataifa ili kuhakikisha wataalamu wa usalama wanakuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto mpya zinazoendelea kujitokeza duniani.
Kozi hiyo imehusisha washiriki 11 kutoka taasisi mbalimbali za usafiri wa anga, wakiwemo washiriki watatu kutoka Mamlaka ya usafiri wa anga ya Uganda, watatu kutoka Zanzibar Aviation Services & Travel (ZAT), watatu kutoka Mamlaka ya viwanja vya ndege Tanzania (TAA) na wawili kutoka Mamlaka ya viwanja vya ndege ya Zanzibar na Pemba. Ushiriki huo umetajwa kusaidia kuimarisha ushirikiano na kubadilishana uzoefu wa kiusalama katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Mafunzo hayo ya siku tano yalifunguliwa rasmi Mei 18, 2026 na Naibu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, Bi. Angela Kabali.
Washiriki wote wametunukiwa vyeti vya kuhitimu mafunzo hayo baada ya kukamilisha ratiba yote ya mafunzo kwa mafanikio.