07/11/2024
LISILOBADILIKA MABADILIKO
Daima naishi kusikia kuwa kuinamako ndiko kuinukako. Je kuinukako bado ndiko kuinamako? Hilo swali tu la balagha. Tuishipo daima lisilobadilika ni mabadiliko. Mengine yote ni mabadiliko yanayobadilika badilika kila kutokeako mabadiliko. Naam, hata miamba hubadilika ikawa mchanga, nyumba ikawa ganjo, miti ikawa mbao, mtu akawa marehemu, mchana ukuwa usiku, giza likawa mwanga.
Hivi nasemani? Naufananisha ulimwengu na jangwa ambapo hapawezi pakachipua lolote. Ila, hata jangwa likinyunyiziwa chemichemi ukuza mazao na kubadili eneo likawa chanikiwiti. Ndipo nikasema lisilobadilika, basi ni mabadiliko tu.
Namaanishani? Tuishipo si ajabu mja kurithishwa taabu na masaibu. Akasalia hana hanani, akiulizwa haungami. Hiyo ndiyo hali halisilia. Kuruba na msukosuko wa maisha ukamkandamiza kiasi cha kujuta kuishi. Akatamani laiti isingekuwa ilivyo. Ila lisilobadilika ni mabadiliko tu.
Kwa hilo, ukirithishwa taabu na masaibu, pambana kubadilisha angalau uwe na mwisho mwema, kwani hata hadithi za Riwaya licha wa muhusika mkuu kuteseka, mara nyingi huishia kwa mwisho mwema. Tupambane
Zaidi ya yote, tusichukiane. Tusisemane vibaya. Tusikadamizane. Tusiumizane. Tusidharauliane. Tusitakiane mabaya. Tusiharibiane mapambano. Daima tusaidiane. Tusisahau kuwa msaada ni kikoa, ukisaidiwa nawe saidia mwingine.
Kesho kwema, kwa vile Jalia yupo.
Mwandisha, mwigizaji,mwanahabari,muhubiri