13/07/2022
SOMO: KUMUONDOA ALIYEKAA KWENYE NAFASI YAKO (Sehemu ya Pili)
BISHOP DR. GODSON ISSA ZACHARIA
KANISA LA UFUFUO NA UZIMA MOROGORO
MHUBIRI: PASTOR CATHERINE AUGUSTINE (AP)
JUMATANO TAREHE 13 JULY, 2022
“Katika shida yangu nalimwita Bwana; Bwana akanijibu akaniweka panapo nafasi”.
(Zaburi 118:5)
Tunamuona Daudi yeye katika shida yake alimuita Bwana na Bwana akamuitikia na kumuweka kwenye nafasi. Kabla ya kumuita Bwana Daudi alikuwa mtu wa huzuni kwa sababu aliondolewa kwenye nafasi yake. Unapoondolewa kwenye edeni yako lazima uwe mtu wa huzuni na mahangaiko. Kuna binti alitakiwa awe ameshaolewa lakini hadi leo anahangaika bado hajaolewa, kuna mama alitakiwa awe na watoto lakini hana mtoto hata mmoja na amekuwa mtu wa huzuni na mahangaiko kwa sababu ameondolewa kwenye nafasi yake.
Unapoondolewa kwenye edeni yako ndipo mateso yanapoanza. Adamu na Hawa walipoondolewa kwenye edeni yao ndipo mateso yalipoanza, Hawa aliambiwa atazaa kwa uchungu na Adamu aliambiwa atakula kwa jasho. Wakati Hawa na Adamu wapo ndani ya edeni mahangaiko hayo hayakuwepo lakini walipotolewa kwenye edeni yao mateso yakaanza. Hivyo ndivyo ilivyo ndoa ilipokuwa shwari mlikuwa mnaitana majina mazuri lakini mlipotolewa nje ya eden ndoa imekuwa ndoano.
Watu leo wanasema vyuma vimekaza lakini wakati huohuo kuna wengine wanapandisha magorofa. Tatizo si vyuma vimekaza bali umeondolewa kwenye nafasi yako na siku ya leo ninakwambia yule aliyemrudisha Daudi kwenye nafasi yake yupo hapa na wewe atakurudisha kwenye nafasi yako kwa jina la Yesu.
“Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala. Akamwambia Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako”(Mwanzo 3:16)
Ni uchawi tu, unarogwa halafu unatengenezewa mtazamo, ukijiangalia unajiona k**a panzi, ukiangalia unaona vyuma vimekaza. Usikubali huo ni uongo wa shetani anataka akutoe kwenye nafasi yako, usikubali kwa jina la Yesu. Tunaondolewa kwenye nafasi zetu kwa sababu bado hatujui majira ya kujiliwa kwetu, tunadanganywa na shetani kuwa sisi ni maskini, sisi ni mapanzi na tunakubali. Siku ya leo nasema usikubali wewe si maskini, wewe si panzi mpasue huyo aliyekaa kwenye nafasi yako kwa jina la Yesu. Ndugu zangu kila mmoja ameondolewa kwenye nafasi yake ingawa tunatofautiana nafasi tulizoondolewa. Mwingine ameondolewa kwenye nafasi ya uzazi, mwingine ameondolewa kwenye nafasi ya kuoa au kuolewa, mwingine ameondolewa kwenye nafasi ya kupata kazi, mwingine masomo lakini habari njema ni kwamba jioni ya leo tutamuondoa yule aliyekaa kwenye nafasi yako na wewe utarudi kwenye nafasi yako kwa jina la Yesu.
Silaha zako zina uwezo hata kuangusha ngome, tumia hizo silaha kumuondoa aliyekaa kwenye nafasi yako, k**a wamekaa kwenye boma lazima bomoa, k**a wamekaa k**a ukuta wa Yeriko bomoa kwa jina la Yesu. Kazi yetu ni kumuondoa shetani na mawakala wake waliokaa kwenye ndoa zetu, biashara zetu, kazi zetu, masomo yetu, uzao wetu kwa jina la Yesu. Hutakiwi kulia kwa sababu umeondolewa kwenye nafasi yako, wewe ni jeshi la Bwana, mwanajeshi anapokuwa vitani anapambana na halii, pambana mpaka urudi kwenye nafasi yako.
Ukiomba hakikisha unaomba haswa kwa sababu aliyekaa kwenye nafasi yako hawezi kuondoka kirahisi. Huwezi kurejesha amani ya ndoa yako kirahisi, huwezi kupata kazi kirahisi, biashara yako haiwezi kustawi kirahisi, unapoambiwa mpige aliyekaa kwenye nafasi yako mpige haswa kwa sababu hana mpango wa kuondoka kirahisi na maandiko yanasema maombi yake mwenye haki yanafaa sana akiomba kwa bidii.
“Kwa kuwa ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye kuheshimiwa, nami nimekupenda; kwa sababu hiyo nitatoa watu kwa ajili yako; na kabila za watu kwa ajili ya maisha yako”.(Isaya 43:4)
Mungu anasema atatoa watu kwa ajili yako ili wakurudishe kwenye nafasi yako. Lakini kuna mashetani wamekaa njiani wanazuia hao watu kukufikia ili kubadilisha maisha yako na wewe kurudi kwenye nafasi yako. Kuna mume wako amezuiwa kuja kwako, kuna kazi ilibidi uipate lakini hujapata, kuna biashara ilibidi umiliki lakini hata mtaji huna kwa sababu shetani na mawakala wake wamewazuia watu wazuri kuja kwako ili wakupatie kazi, biashara. Leo tutampasua huyo shetani na mawakala wake na wewe utarudi kwenye nafasi yako kwa jina la Yesu. Usisubiri utabiriwe na nabii ili urudi kwenye nafasi yako, wewe piga majeshi usiku na mchana hadi shetani aachie mume wako, mke wako, watoto wako, kazi yako, biashara yako, masomo yako na urudi kwenye nafasi yako kwa jina la Yesu.
KWA MSAADA ZAIDI NA MAOMBEZI:
FIKA KANISANI,
KANISA LA UFUFUO NA UZIMA MKUNDI MINARA MITATU MOROGORO
AU WASILIANA NASI KUPITIA
FACEBOOK: Pastor Dr Godson Issa Zacharia
Follow us on INSTAGRAM: pastordrgodson
Follow us on YOUTUBE: Pastor Dr. Godson Zacharia
TEL: +255 719 798 778
BLOG: Ufufuo na Uzima Morogoro
http://ufufuonauzimamorogoro.blogspot.com/
11/07/2022